31 December 2005

Bi Lucy Kibaki atufungia mwaka.



Nimemchagua Bibi Lucy Kibaki kutufungia mwaka, sijui wenzangu mnasemaje kuhusu uteuzi huu.. kama hamjaridhika msisite kutoa malalamiko yenu. Ndiye huyo katika picha.

26 December 2005

Kibanda cha majadiliano ya neno blogu kwa kiswahili.

Wasomaji na wanablogu wote, ili kufanikisha zoezi la upatikanaji wa neno blogu kwa kiswahili, nimeona niweke kiungo ambacho sisi wote tutakuwa tunakutanikia, Kaka Ndesanjo alitoa wazo hili na Kaka Mwandani akatoa kiungo hiki kwa Kaka Jeff, Da Mija akakibandika. Kiungo hiki ambacho kina kichwa cha habari "BUNGABONGO YA NENO BLOGU KWA KISWAHILI" nimekiweka upande wa kulia juu ya Kichwa cha habari "Blogu Motomoto". Ingekuwa ni vyema basi yale yote tuliyoyapendekeza tuyahamishie huko kibandani.

23 December 2005

Viti Maalumu ...

Jamani sijui kama na wenzangu mnaliona hili, binafsi ninaona kuna njama za chini kwa chini zinazofanywa na wanaume kuwazima kabisa wanawake katika harakati za ukombozi. Kumkamilishia mtu mahitaji yake ni kumfanya mtu asipambane, na bila mapambano hakuna ushindi, ushindi utabaki kwa yule anayekupigania. Hii tabia ya kutoa viti maalumu kwa wabunge wanawake inatufanya tusiwajibike ipasavyo na kubakia pale pale. Viti hivi vilitakiwa vipiganiwe ili utakapokipata ujue kweli jinsi ya kukifanyia kazi na kukiwajibikia. Hii tabia ya kupewa-pewa ina mambo mengi ambayo wanawake tunatakiwa tuyajue...Kupewa kwa aina yoyote ile kunaendana na kulipa fadhira, kwa hiyo kupewa huku kwa viti maalum tusikuchukulie juu juu, wabunge hawa wajiandae kupangiwa ya kufanya na kuwekewa mipaka ya kufika. Na kama ukitaka kwenda kinyume na mipaka hiyo basi utakumbushwa jinsi ulivyokipata kiti, kwa hiyo itabidi ukubali yaishe.

Sasa wenzangu hali hii kweli itatufikisha tuendako? ..hili nalo ni lazima tulifanyie kazi. Wabunge wenyewe waliotangazwa hawa hapa chini.

2005-12-23 08:32:50
Na Mwandishi wetu.


Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imewatangaza rasmi wanawake 64 wa Vyama vya CCM na CHADEMA kuwa wabunge wa viti maalum.
Wabunge 58 miongoni mwa hao ni wa CCM na wengine sita ni wa CHADEMA.

Hata hivyo taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ilisema tume imeshindwa kutangaza wabunge maalum kupitia chama cha CUF kwa sababu chama hicho hakijawasilisha majina.

Taarifa hiyo iliwataja wabunge wa viti maalum kupitia CCM kuwa ni Bi Anna Magreth Abdallah, Bi Faida Mohamed Bakari, Bi Martha Jachumbulla, Bi Elizabeth Nkunda Batenga, Bi Zainabu Matitu Vulu na Bi Cynthia Hilda Ngoye.

Wengine ni Bi Esther Kabadi Nyawazwa, Bi Mariam Salum Mfaki, Bi Anastazia James Wambura, Bi Gaudensia Mugosi Kabaka, Bi Sijapata Fadhili Nkayamba, Dk. Aisha Omari Kigoda, Bi. Salome Joseph Mbatia na Dk Lucy Sawere Nkya.

Hali kadhalika Bi Joyce Nhamanilo Machimu, Bi Eliata Ndumpe Switi, Bi Lediana Mafuru Mng’ong’o, Bi Diana Nkumbo Chilolo, Dk Batilda Salha Burian, Bi Asha Mshimba Jecha na Bi Fatma Othman Ali.

Katika orodha hiyo ya wabunge wa CCM pia kuna Bi Devota Mkuwa Likokola, Bi Bahati Ali Abeid, Dk Maua Abeid Daftari, Bi Fatma ABdallah Mikidadi, Bi Janet Bina Kahama, Bi Aziza Sleyum Ally, Dk Asha-Rose Migiro, Bi Shamsa Selengia Mwangunga, Bi Margreth Agnes Mkanga, Bi Zuleikha Yunus Haji na Bi Lucy Thomas Mayenga.

Wengine ni Bi Amina Chifupa Mpakanjia, Bi. Margreth Simwanza Sitta, Bi Felista Aloyce Bura, Bi Halima Mohamed Mamuya, Bi. Rosemary Kasimbi Kirigini, Bi Mwanne Ismail Mchemba, Bi Anna Richard Lupembe, Bi Halima Omari Kimbau, Bi Dorah Herial Mushi na Bi Mwantumu Bakari Mahiza.

Wabunge wengi wa CCM wa viti maalum vya wanawake ni Bi. Riziki Lulida Said, Bi Mariam Reuben Kasembe, Bi Mwanakhamis Kassim Said, Bi. Janeth Mourice Massaburi, Bi Benadetha Kasabogo Mushashu, Bi. Maida Hamadi Abdallah, Bi Mwaka Abdulrahman Mbaraka, Bi Kumbwa Makame Mbaraka, Bi Joyce Martin Masunga, Bi Josephine Johnson Ngenzobuke, Bi Kidawa Hamid Salehe, Bi Martha Moses Mlata, Bi Shally Joseph Raymond, Bi Maria Ibeshi Hewa, Bi Pindi Hazara Chana na Bi Stella Martin Manyanya.

Kwa upande wa CHADEMA waliotangazwa kuwa wabunge wa viti maalum vya wanawake ni Bi Grace Sindato Kiwelu, Bi Maulidah Anna Komu, Bi Mhonga Said Ruhwanya, Bi Lucy Fidelis Owenye, Bi Susana Anselm Jerome Lyimo na Bi Halima James Mdee
Kuhusu wabunge wa CUF Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema imechukua hatua za kukiomba chama hicho kuwasilisha majina.

’Baada ya CUF kuwasilisha majina na taratibu zinazotakiwakuzingatiwa Tume itawatangaza wabunge wa viti maalum kupitia chama cha CUF,’ilisema taarifa.

SOURCE

16 December 2005

Kuhusu neno "Blog" kwa kiswahili.

Kwanza kabisa labda nianze hivi..."Jambo haliwi jambo hadi uliamuru kuwa jambo ndipo hugeuka kuwa jambo". Kwa kipindi sasa wanablogu tumekuwa tukijitahidi kutafuta neno blog kwa kiswahili ili kuendelea kuikuza lugha yetu. Lakini kwa bahati mbaya mbio hizi zimekuwa zikizorotazorota kutokana na sababu mbalimbali. Pamoja na sababu zote zinazozorotesha upatikanaji wa neno blog katika kiswahili, nimekuja kugungua kwamba iliyo kubwa kabisa ni hii.." Tumejifunga wenyewe"...kwamba tunatafuta maneno ambayo yapo tayari, na tena yanayoendana na maana halisi ya neno blog. Sikatai kwamba ni njia isiyofaa, lakini tukumbuke kwamba ..Fasihi yoyote huzaliwa, hukua, na hufa. Na kama ni hivyo basi kwa nini wanablogu tusizae neno letu wenyewe na sisi ndio tukaliamuru hilo neno kuwa na maana ya Blog kwa kiswahili, ila katika uzazi huo tuzingatie Kanuni za lugha, kwamba ni lazima liweze kutamkika vizuri katika nafsi ya kwanza, ya pili na ya tatu, na katika nyakati zote, wakati uliopo, uliopita na ujao.
Mfano neno NGWANGA. Hili neno halina maana yoyote, lakini kuanzia sasa ninaliamuru liwe na maana ya blog. Neno hili limetimia katika nafsi na nyakati za kiswahili.

Mfano... Ninaenda kungwanga.
.........Unaenda kungwanga.
.........Anaenda kungwanga.

Najua wasomaji bado mnasitasita, lakini hebu fikirieni majina ya vitu vilivyopo hapa ulimwenguni, je yanahusiana na maana ya vitu vyenyewe?? hapa ukubali usikubali jibu ni hapana. Na kama jibu lingekuwa ndiyo, basi vitu vyoote hapa duniani vingekuwa na jina moja.

Hakukuwa na ulazima wowote wa NYUMBA kuitwa nyumba, au kinu kuitwa kinu, au dunia kuitwa dunia au kitabu kuitwa kitabu. Ni watu walikaa na kuamua hiki kiitwe hivi na hiki vile. Na kama tunavyojua fikra hujenga taswira, baada ya neno Nyumba kuanza kutumika kuwakilisha jengo basi taswira nayo ikajengeka akilini..Nyumba ni jengo. Na ukienda kwa waingereza wenyewe jengo ni HOUSE.

Kwa hiyo kwa mtazamo wangu naona tusiendelee kupoteza muda, tupeane zoezi la kila mwanablogu kuleta maneno mawili mapya kabisa, halafu tutapiga kura na kuchagua moja.
Na kumaliza mchezo. Tukifanikiwa kulitekeleza hili tutakuwa na faraja kubwa kwani tutakuwa tumefanikiwa kuumba na kutia pumzi. Msangi Mkubwa ameianzisha tena mada hii, msome na usome maoni ya wengine.

11 December 2005

NANI ZAIDI??



Nimekuwa nikijaribu kuilinganisha miamba hii miwili ili nimpate nani ni zaidi, lakini nimeshindwa kupata jibu. Sasa wasomaji naomba mnisaidie. Siku za nyuma nilipandisha undani wao, lakini kama hukuweza kupata muda wa kuupitia unaweza ukasoma hapa na hapa.

Haya tena makubwa!!!

Leo nikiwa katika harakati zangu za kusasambua habari mtandaoni nikakutana na shairi hili hapa. Hii sasa hatari hii.

08 December 2005

..".WABARIKI VIONGOZI WAKE"...MtiMkubwa umetoa tena dukuduku lake!

MtiMkubwa kama kawaida yake umetoa tena dukuduku lake hili hapa chini.

"Miye naupenda sana wimbo wa Taifa wa Tanzania (Mungu Ibariki Afrika). Wimbo huu siye Watanzania tumeukopa toka Afrika ya Kusini. Nyimbo hii ni nzee sana ilitungwa kunako mwaka 1897 kwa hiyo una miaka takribani mia moja na kumi na moja! (111)! Muziki wa nyimbo hii ni utunzi wa Hayati Enoch Sentonga, ambapo maneno yake yaliyotungwa na Hayati Enoch Sentonga na baadaye yakaja kukarabatiwa na Mshairi Samuel Mghayi. Wimbo hatujaukopa Watanzania tu, na Wazambia nao na Wazimbabwe hali kadhalika. Lakini sijui ni kwa sababu gani Wazimbabwe waliuacha wimbo huu na kuchukua mwingine.

Wimbo huu huwa unanipa na kunitoa raha pale unapofika kwenye mstari wa "WABARIKI VIONGOZI WAKE"! Ukifika hapo huwa unanikumbusha sura za viongozi walionuna wakiwa wamesimama pale mein stend, neshno stedium, Huku askari wa vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na chipukizi wa chama wakiwa wamekauka juani na saluti kali. Halafu na Watanzania wapenda amani na utulivu, Wafanyakazi, Wakulima na "Wazururaji" wakiwa wametanda kwenye sehemu zingine za uwanja wakishiriki kwenye hiyo ghafla aidha kwa ridhaa zao au vinginevyo. Miujiza ya Tanzania Mei Dei au SabaSaba wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na hai-skuli wote wanashiriki kikamilifu.

Turudi kwenye Mungu Ibariki Afrika, hususani pale kwenye mstari wa "WABARIKI VIONGOZI WAKE". Hapo nadhani ndipo Watanzania tulipopewa uwezo wa pekee wa kuweza kumtia kizunguzungu Mwenyezi MUNGU! Maanake Mwenyezi Mungu akiwatazama hao viongozi tunaomuomba awabariki, Mwenyezi Mungu mwenyewe anapata kizunguzungu. Lakini dua letu sio kama linaishia kwa viongozi wetu wa Tanzania peke yake, bali tunawaombea na majirani zetu kama Waganda wakati ule wakiwa na Idd Amini Dada, Malawi na Dr Hasting Kamuzu Banda, Zaire na Mobutu Sese Seko Kuku Mbwendu wa Zabanga, Viongozi wazalendo wa Wahutu na Watutsi wa Rwanda na Burundi, kina Alphonso Dhlakama kiongozi wa chama cha RENAMO cha Msumbiji. Dua zetu pia zilikuwa zinawaombea kina Eyadema, Omar Bongo,Paschal Lisouba, Jean Babtist Bokassa, Macias Nguema, Mfalme Hassan, Jaffar Nimeir, Omar Bashir na Hassan Tourabi, John Voster, Tommy Ndabaningi Sintole, Abel Muzorewa, Morgan Tsivangirai, Jonas Savimbi, Gatsha Mongasuthu Buthelezi na wengineo wote wamo kwenye dua hiyo ya "WABARIKI VIONGOZI WAKE".

Leo 09 disemba Watanzania tutaimba tena MUNGU IBARIKI AFRIKA, WABARIKI VIONGOZI WAKE,...Wakati tukiimba hivyo tutazame jirani yetu Kenya. Tumuombe Mwenyezi Mungu AWABARIKI VIONGOZI WAKE. (Kuna neno nimetaka kulisema lakini nimelimezea) kama hapo chini.
BONYEZA HAPA upaone hapo chini.

07 December 2005

Jamani ninaomba ruksa yenu!

Ndugu wasomaji, Kuna hili suala nyeti sana katika ulimwengu huu, suala la MAHUSIANO YA KIMAPENZI. Suala hili ingawa ni nyeti sana na linalomhusu karibu kila mtu mzima hapa ulimwenguni, lakini ni suala la mwisho kabisa katika kuzungumziwa kwa UWAZI, imekuwa ikioneka kama ni ukosefu wa adabu kulijadili hadharani, Matokeo yake watu tumekuwa tukilivamia tu bila kuchukua tahadhari zozote au bila kujua tunacho kihitaji hasa katika mahusiano hayo na hivyo kusababisha wengi wetu kuishia matatizoni.

Binafsi nimekaa nikaona si vyema kuendelea kulifungia macho suala hili, kuna haja ya kuanza kulizungumza kwa uwazi huku wote kwa pamoja tukishirikiana katika kubadilishana mawazo. Nia hasa ikiwa ni kufunguana akili ili tuweze kuwa makini zaidi wakati tunapoamua kuingia katika mahusiano hayo.

Hivyo basi sina budi kuomba ruksa yenu ili kwa pamoja tukubaliane kuliweka sebuleni jambo ambalo ambalo linaonekana ni la chumbani.

Kuna mambo mengi ya kuyajadili, lakini labda tuanze na hili dogo.

NI VITU GANI MWANAUME HUTEGEMEA KUVIPATA KUTOKA KWA MWANAMKE? NA MWANAMKE KUTOKA KWA MWANAUME?

Wasomaji, ninaamini mjadala huu utatusaidia katika kujitambua zaidi, na kuwa makini wakati tunapotaka kufanya maamuzi.

04 December 2005

Gertrude Ibengwe Mongella.

Kama kuna wanawake wa kitanzania ambao wameweza kuionyesha dunia kwamba Tanzania nayo ina wanawake wa shoka, basi Mama Gertrude Mongella naye yumo tena katika namba ya juu, hakosi katika namba tatu bora za mwanzo...nani anabisha? Mama huyu ambaye ni mwanasiasa, mwalimu, mwanaharakati, mke na mama wa watoto wanne, ndiye yule aliyeuongoza mkutano wa nne wa dunia kuhusu wanawake uliofanyika Beijing China mwaka 1995. Na ni huyu huyu ambaye ni rais wa kwanza wa bunge la afrika lililoundwa mwaka 2004. Ndugu wasomaji wangu naomba mjue kwamba bunge hili si la kina mama peke yake, ni bunge mchanganyiko. Kwahiyo mwanamama huyu kitendo cha kuwabwaga wanaume wote wa Afrika tena katika uchaguzi wa mara ya kwanza si kitu masihara kabisa.

Kabla sijaendelea zaidi kuwapasha juu ya mambo ambayo mama huyu ameshawahi kuyafanya, ningependa niwadokeze kidogo juu ya maisha yake binafsi.

Mama Gertrude Mongella alizaliwa katika kisiwa cha Ukerewe, mkoani Mwanza mwaka 1945 akiwa ni mmoja kati ya watoto wanne katika familia yao. Baba yake Patrice Magologozi alikuwa ni mjenzi, fundi seremala na mwanaharakati akikabiliana na siasa za mkoloni. Mama yake Bibi Nambona alikuwa ni mkulima stadi. Alizaliwa kipindi ambacho ubaguzi kati ya watoto wa kike na wakiume katika jamii yao ulikuwa umeshika hatamu, wanawake walizuiliwa mambo mengi, mfano kuongea mbele ya wanaume, kula vyakula baadhi ya vyakula au sehemu zilizonona za nyama, mfano mapaja ya kuku,firigisi mayai na vinginevyo vingi. Gertrude aliliona hili na rohoni mwake hakukubaliana nalo kabisa, lakini anamshukuru sana baba yake ambaye alikuwa akimtia moyo na kumwambia asifungwe na hizo mila na desturi ale anachotaka, aseme anapoona pana ukweli na shule atakwenda.

Alipokuwa na umri wa miaka 12, alianza shule iliyokuwa ikiendeshwa na watawa wa Maryknoll Nuns, Shule hii ilikuwa na malengo ya kuwaelimisha na kuwanyanyua watoto wa kike. Na hii ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kusafiri toka azaliwe.

Baadaye alijiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam ambako alipata Shahada ya elimu. Mwaka 1975 aliingia katika siasa na kuwa mwanachama katika Baraza la kutunga sheria la Afrika Mashariki (EALA).

Tangu wakati huo, amekuwa akishikilia nafasi nyingi za uongozi katika Chama tawala na Serikali ya Tanzania, na nje ya nchi bonyeza hapa usome mwenyewe. Na kwa baadhi ya mahojiano ambayo amekwisha yafanya bonyeza hapa na hapa usome, na hapa umsikilize.

Watanzania hatuna budi kushukuru kuwa na mwanamke jasiri na muwezaji wa mambo kama huyu. Gertrude Mongella ni mtu asiye tishika na ndio sababu hata dunia imeweza kumuona. Na baada ya kumfuatilia sana nimegundua jambo moja, si mtu anayekurupushwa na matokeo ya jambo, ni mtu anayeangalia nini kiini au chanzo cha jambo hilo. Mfano ni pale alipozungumzia ya umaskini na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika bara la Afrika. Alisema kwamba" hebu tujiulize waafrika wengi wanaopigana utakuta wanamiliki silaha bora na za gharama mno, lakini mwafrika huyo huyo hana pesa hata ya kuweza kumnunulia mwanae kalamu!! Sasa hapo ujue lipo jambo.. ninani anayempa mwafrika huyu hizo silaha?? ..huyo ndiye wa kusakamwa kwani kama angekuwa na nia nzuri basi angempa kalamu au nyenzo za kufanyia kazi. Hebu usiache kumsikiliza katika kiungo nilichokuwekeeni hapo juu.

Zidumu fikra za Mama Mongella.