14 August 2005

Oprah Winfrey.

Kila penye juhudi mafanikio hutokea. Mwanamama Oprah ni mfano halisi wa msemo huu. Huyu ni mmarekani mweusi aliyezaliwa 29/01/1954 huko Kosciusko Mississippi katika familia ya kimaskini kabisa. Baba yake Vernon Winfrey na mama yake Vernita Lee hawakuwahi kuoana,walimpata Oprah wakiwa ni marafiki tu baba akiwa na miaka 20 na mama 18. Baba yake alikuwa akifanya kazi mjini na alipopata rikizo alikuja kijijini kwao kutembea ndipo alipokutana na Vernita Lee na kufanya urafiki. Likizo ilipokwisha Vernon alirudi kazini, hawakuwasiliana tena hadi baada ya miezi tisa,pale alipopokea barua kutoka kwa Vernita yenye maneno machache sana na ya kujieleza LETE NGUO, MTOTO AMEZALIWA. Na huu ndio ulikuwa mwanzo wa Oprah, baada ya hapo mama yake alihamia mjini Milwaukee kutafuta kazi na kumwacha Oprah shamba akilelewa na bibi yake. Huko bibi yake aligundua kuwa mjukuu wake kuwa ana akili sana hivyo akaanza kumfundisha kusoma, amini usiamini Oprah ameanza kujua kusoma akiwa na umri wa miaka miwili, na katika umri huo huo kila jumapili alipokuwa akienda kanisani alipewa wasaa wake kusimama mbele ya kanisa na kuimba mashairi, ama hakika kijiji chote walimjua kwamba ni mtoto alije na kipaji cha pekee.

Alipokuwa na umri wa miaka 6, mama yake alimchukuwa na kwenda kuishi naye Milwaukee, huko mambo hayakwenda vizuri kabisa kwani mama yake hakuwa na muda wa kumjali kutokana na kutoshinda nyumbani kwa ajili ya kazi, yeye ndio alifanywa mlezi wa wadogo zake na hakupendwa kama wenzie, alipokuwa na miaka 9 alibakwa na mmoja wa binamu zake ndani walipokuwa wakiishi, na haikuishia hapo rafiki zake na mama yake walimfanyia hivyo pia bila mama yake kujua. Oprah hakuelewa nini kilikuwa kikiendelea maishani mwake hivyo akaanza ukorofi usiowezekana, alianza wizi wa vitu vya mama yake, alianza kutumia madawa ya kulevya na kushinda maskani. Mama yake alimshindwa na kuamua kumpeleka jela ya watoto wa watukutu baada ya Oprah kutoweka nyumbani kwa wiki mbili, bahati nzuri kwa Oprah jela hiyo haikuwa na nafasi na ndipo mama yake alipoamua kumpeleka kwa baba yake.

Oprah alianza kuishi na baba yake alipokuwa na miaka 14, na huu ndio ulikuwa mwanzo mpya kwa oprah kwani baba yake alikuwa ni mkali kupindukia, lakini pamoja na hayo Oprah alimalizia tukio la mwisho la kupata mimba katika umri huo huo wa miaka 14 na kuzaa mtoto wa kiume katika mwezi wa saba, mwanae alifariki baada ya wiki mbili. Baada ya tukio hilo na kasheshe alilolipata kutoka kwa baba yake, Oprah aliona katika nyumba ya baba yake hakuna mchezo ni lazima kutii. Baba yake alimpangia ratiba ya kusoma ambayo ilimbana asiweze kupata muda wa kufanya utundu wake, alitakiwa kila wiki amalize kusoma kitabu kimoja na kuwasilisha muhtasari kwa ufupi wa kitabu kizima, na si hayo tu alitakiwa pia ajifunze misamiati mitano kila siku ya Mungu na aliposhindwa kufanya hivyo siku hiyo alilala njaa. Anasema katu baba yake hakukubaliana na matokeo ya chini ya mitihani ya Oprah ambayo anajua kabisa mwanae ana uwezo nayo. Anasema siku moja alileta matokeo yenye C'nyingi nyumbani siku hiyo baba yake alimkalisha chini kwa upole na upendo na kumweleza kwamba ni marufuku kuleta C katika nyumba ile bali A, akaendelea kumweleza kwamba si kwamba anamlazimisha kupata kitu ambacho Oprah hana uwezo nacho, bali ni kitu kilicho dhahiri kwamba uwezo wake uko katika A na sio C. Kuanzia hapo Oprah anasema alipata nguvu ya kujiamini kwamba anaweza, na tangu hapo alikuwa ni mwanafunzi wa kupata A tupu. kutokana na uwezo wake wa kimasomo na kujiamini, alichaguliwa kuwa rais wa wanafunzi na katika kipindi hicho hicho alichaguliwa kuwa mmoja kati ya wanafunzi wawili katika kila state kwenda kushiriki mkutano wa vijana ikulu na ni huko ndiko mambo yake yalikoanza kumchanganyia kwani alipata nafasi ya kufanyiwa mahojiano na redio ya huko, alifanya mahojiano vizuri sana kiasi kwamba wakampa kazi ya utangazaji. Kipindi hiki Oprah alikuwa na miaka 17 hivyo alianza kazi huku akisoma, anasema ilibidi aongeze juhudi ya ziada ili kuweza kumudu kazi na masomo. Na kadri siku zilivyokuwa zikiendelea mafanikio yake yalizidi kuongezeka, alitoka kwenye radio na kuingia katika luninga na ni huko ndiko alikoweza kuazisha kipindi chake mwenyewe cha Oprah Winfrey show, na hakuishia hapo sasa hivi anamiliki studio yake mwenyewe ya filamu na habari. Kwa ufupi ni bilionea na kuna hati hati ya kuwa rais wa baadaye wa Marekani. Naomba Mungu awe baada ya Bush. Mungu na azidi kumbariki mwana mama huyu.