31 January 2006

Nani Zaidi......

Bado najiuliza sijui kwa nini MtiMkubwa anaogopa kufungua blogu yake, majuzi amenitumia waraka huu ili wote tujadili kihoja hiki cha wabunge...haya endelea hapo chini.

"Kuna wakati nikikaa nikawaza mambo ya Watanzania nashindwa kupata jibu. Leo nimefikwa na jambo ambalo nimeshindwa kupata jibu. Kwa wale wenye nafasi naomba msomee habari hiyo hapo chini halafu mnisaididie majibu: Maswali niliyojiuliza "..Kati ya mbunge na daktari nani anastahili kulipwa mshahara mkubwa?..Halafu Mheshimiwa Kimiti anaposema "..madai yao yanatokana na ukweli kuwa wabunge wana majukumu mengi na makubwa ya kuwahudumia watu kuliko watumishi wengine wote.." Kama ni kweli?

Wabunge wataka kukata ’keki’ zaidi ya taifa

2006-01-26 08:38:24
Na Mashaka Mgeta

Baadhi ya Wabunge wamechachamaa na kuitaka serikali iwaongezee mishahara, posho na marupurupu ili kuwawezesha kuwatumikia wapiga kura wao kwa ufanisi zaidi.

Lakini kwa upande mwingine wametaka madai hayo hayo yasiandikwe au kutangazwa katika vyombo vya habari, kwa maelezo kuwa zitachochea hisia mbaya na kuwafanya wasikubalike kwa wapiga kura wao.

Wabunge hao walitoa mapendekezo hayo jana walipokuwa wakichangia mada kuhusu masharti ya Mbunge iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Philemon Luhanjo katika semina ya mafunzo inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Bw. Luhanjo aliwaonya wabunge dhidi ya madai yao hayo na kuwataka wazingatie maslahi yanayokidhi matakwa ya usawa kwa wananchi wote katika kugawana pato la taifa linalotokana na vyanzo mbalimbali zikiwemo shughuli za uzalishaji mali zinazofanywa na wananchi.

Alisema hatua ya kudai maslahi bora zaidi kuliko ya watumishi wengine, ni sawa na kuonyesha ubinafsi aliouita kuwa ’collective selfishness’.

Akichangia mada hiyo, Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Bw. Paul Kimiti alisema madai yao yanatokana na ukweli kuwa wabunge wana majukumu mengi na makubwa ya kuwahudumia watu kuliko watumishi wengine wote.

Bw. Kimiti aliwaonya wabunge wasilichukulie mzaha dai hilo wala kulionea aibu kwa kuwa ni miongoni mwa masuala nyeti yanayowahusu.

Mbunge huyo wa siku nyingi, alisema suala la kudai maslahi bora kwa wabunge liliwahi kufanyika pia mwaka 1980 ambapo Spika wa sasa, Bw. Samwel Sitta, Naibu Spika, Bi Anna Makinda na yeye (Kimiti) walikuwa miongoni mwa wabunge waliokuwa kwenye kundi la kudai maslahi hayo.

Hata hivyo alisema madai hayo yalitoweka baada ya wajumbe kadhaa wa kundi hilo ’kutunukiwa’ Uwaziri katika serikali ya awamu ya pili.

Bw. Kimiti alisema madai hayo ni muhimu kwa wabunge kwa vile Wakuu wa Mikoa wanapata kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya shughuli za hamasa zenye mwelekeo wa kisiasa kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Bw. Kimiti, hivi sasa wabunge wanapata mshahara wa Sh milioni 1.2 na kiasi kingine cha takribani Sh milioni moja kila mwezi kwa ajili ya kufanikisha huduma jimboni, fedha ambazo hazihusiani na posho na marupurupu mengine wanayoyapata kwenye vikao vya bunge, vikao vya mabaraza ya madiwani na wanapokuwa safarini.

Naye Naibu Waziri wa Elimu Bw. Ludovic Mwananzila alisema hatua ya wananchi kulalamika wakati wabunge wanapodai ongezeko hilo inatokana na uelewa wao mdogo walionao kuhusu wajibu wa Mbunge.

Bw. Mwananzila alisema uelewa kama huo unachochewa na waandishi wa habari wanapoandika ama kutangaza habari zinazohusu madai ya ongezeko la maslahi ya wabunge, na hivyo kuwafanya (wabunge) wasikubalike kwa wapiga kura.

Alisema kutokana na hali hiyo, habari zinazohusu madai ya wabunge kutaka ongezeko la mishahara, posho na marupurupu hazipaswi kuwafikia waandishi wa habari wala kutangazwa au kuandikwa kwenye vyombo vya habari.

Pia Bw. Mwananzila aliiomba serikali kutoa waraka maalum wenye lengo la kuwashawishi wananchi waamini kuwa posho za wabunge ni kwa ajili ya matumizi kama vile ya kununua mafuta ya magari yao na siyo vinginevyo.

Naye Mbunge wa Iramba Mashariki, Bw. Mgana Msindai alisema alisema ongezeko hilo ni muhimu kwa vile litakuwa linakidhi mahitaji yao.

Bw. Msindai aliyataja baadhi ya mahitaji hayo kuwa ni kulala kwenye hoteli zinazostahili wanapokuwa kwenye misafara ya Mawaziri wanaposafiri ndani ama nje ya nchi na kuwa na magari yenye hadhi isiyopungua Sh milioni 50.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bahi Bw. William Kusila alisema wabunge ni hazina ya ufumbuzi wa matatizo ya wananchi hivyo wanapaswa kupata ongezeko la mishahara, posho na marupurupu.

Katika kuchangia hoja hiyo, Bw. Kusila aliwahimiza wabunge wapya kuunga mkono madai ya kuongezewa posho, mishahara na marupurupu ili wamudu kuwahudumia wapiga kura wao vinginevyo wasitarajie kuchaguliwa tena.

Bw. Kusila alisema watu wanaopinga hoja za madai ya ongezeko hilo wana kile alichokiita ’wivu wa jumla’ na kwamba hawana mapenzi mema na wabunge.

Naye Mbunge wa Rufiji, Profesa Idrissa Mtulia alisema wabunge na familia zao, wanastahili kutibiwa kwenye hospitali zenye hadhi ili kupata huduma mapema na hivyo kuwa na wakati mzuri wa kurejea kwa wapiga kura wao.

Hata hivyo, mbali na kuwataka wafikirie kuhusu haki ya mgawanyo sawa wa pato la taifa, Bw. Luhanjo aliwahakikishia wabunge hao kuwa, pamoja na mambo mengine serikali itazifanyia kazi hoja zao.

24 January 2006

Hadi lini Wachina wataendelea hivi?..MtiMkubwa ahoji...

Watanzania wenzangu,

Miezi kadhaa iliyopita niliwatumieni taarifa niliyoinukuu kutoka katika gazeti la Nipashe iliyokuwa na kichwa cha habari "..Mchina Amtwanga Hedi Mbongo na Kuzirai.." Leo swahiba wangu Dennis Londo kanitumia habari nyingine kama hiyo lakini sasa ni ya mauaji.

Habari kamili hiyo hapo chini:


Mchina mbaroni kwa mauaji ya mfanyakazi mwenzake Mtanzania Ni katika mradi wa maji ya Ziwa Victoria Na Anthony Komanya, ShinyangaMCHINA anashikiliwa na polisi mkoani Shinyanga kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mfanyakazi mwenzake Mtanzania.Raia huyo China, Yuan Yan Bin (42), mfanyakazi wa Shirika la China Civil Construction Corporation, anatuhumiwa kusababisha kifo cha mfanyakazi mwenzake kwa kumgonga na gari kwa makusudi Jumanne iliyopita, akimtuhumu kwa wizi wa dizeli.Kaimu Kamanda wa polisi mkoani wa Shinyanga , Karibueli Shoo, amemtaja aliyefariki kwa kugongwa na gari kuwa ni Benson Msengi (28) aliyekuwa ameajiriwa na shirika hilo, akiwa dereva wa tingatinga la uchimbaji.Shoo alisema Yan Bin, ambaye hivi sasa amelazwa katika hospitali ya mkoa akiongezewa maji kwa njia ya dripu, atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.Habari kutoka kwenye eneo la tukio zilizotolewa na baadhi ya wafanzakazi wa shirika hilo walioshuhudia tukio hilo, zinadai kuwa raia huyo wa China, akiwa na wafanyakazi wengine, siku hiyo walimshambulia Msengi kwa kumpiga nondo baada ya kumtuhumu kuiba dizeli.Mmoja wa wafanyakazi ambaye amekwishatoa maelezo polisi, lakini hakutaka jina lake litajwe, alidai na yeye alishambuliwa na watu hao alipojaribu kumsaidia marehemu wasiendelee kumtesa.Alidai baada ya kumpiga sana, Wachina hao walimfunga marehemu kamba mikono kwa nyuma, wakamtupa kwenye gari Nissan ‘pickup’ na kuelekea kwenye kambi kuu, karibu na mjini Shinyanga.Mwingine anayesemekana kushuhudia tukio siku hiyo ni katibu wa mkoa wa chama cha wafanyakazi katika shirika la STAMICO, Simon Kafula, ambaye alikuwa hapo kambini kwa masuala ya wafanyakazi.Kafula anadai aliona Yan Bin alivyoendesha na kumgonga kwa makusudi marehemu akiwa bado amefungwa kamba walipowasili kwenye kambi hiyo ya Lubaga.Polisi jana ilithibitisha pia kwamba Kafula amekwishatoa maelezo kituo cha polisi mjini hapa.Baadhi ya wafanyakazi, wakielezea chanzo cha tukio, wamedai siku hiyo wakiwa kwenye Mlima wa Old Shinyanga, panapojengwa tanki kuu la maji ya mradi wa kufikisha maji Shinyanga, walionekana watu wawili kwa mbali wakiwa na madumu ndipo inadaiwa Yan Bin aliagiza wafanyakazi, akiwemo Msengi, kuwakimbilia watu hao.Hata hivyo, watu hao walifanikiwa kutoweka wakiacha madumu mawili matupu nyuma ambayo wafanyakazi hao, akiwemo Msengi, waliyapeleka kwa Yan Bin.Mmoja wafanyakazi hao alidai Msengi alipokwenda kukabidhi funguo za tingatinga kwa Yan Bin ili aende kupata chakula cha mchana ndipo alipoanza kushambuliwa.Inadaiwa Yan Bin alianza kumshambulia kwa kumpiga na nondo sehemu mbalimbali za mwili na kuungwa mkono na Wachina wenzake wapatao sita ambao walimshambulia kwa kutumia mipini ya sepetu na koreo.Inasemekana mmoja wa wafanyakazi alijaribu kumsaidia marehemu, lakini akajikuta anashambuliwa na Wachina hao na kufukuzwa asitoe msaada mpaka walipomweka ndani ya gari na hatimaye kufariki dunia

22 January 2006

Siti binti Saadi.


Kama isivyowezekana kutenganisha kalamu na wino, basi ndivyo isivyowezekana kumtenganisha Siti binti Saadi na muziki wa Taarabu.

Siti binti Saadi alizaliwa katika kijiji cha FumbaTanzania visiwani 'Zanzibari' mwaka 1880. Alipozaliwa alipewa jina la 'Mtumwa' hii ni kwa vile alizaliwa katika kipindi cha utumwa wa kiarabu. Jina la Siti alipewa na mkabaila mmoja wa kiarabu likiwa linamaanisha 'Lady' kwa kiingereza.

Baba yake bwana Saadi alikuwa ni Mnyamwezi kutoka Tabora na mama yake alikuwa ni Mzigua toka Tanga, lakini wote wawili walizaliwa Zanzibari. Hali ya maisha ya familia yao ilikuwa ni duni sana na walijishughulisha zaidi katika shughuli za kilimo na ufinyanzi kazi ambazo Siti alijifunza na kuzimudu vizuri pia.

Kama waswahili wasemavyo 'kuzaliwa masikini si kufa masikini' Siti alibarikiwa kuwa na kipaji cha pekee cha uimbaji. Kipaji hiki kilimsaidia sana tangu siku za awali za maisha yake kwani alitumia uimbaji wake kuuza vyungu vya mama yake alivyokuwa akimsaidia kuvitembeza. Siti alipoimba sauti yake iliweza kupaa na kusafiri kwa umbali wa maili nyingi na hii ndio ilikuwa ishara ya watu kujua kwamba vyungu vya kina Mtumwa vinapita leo. Alifananishwa kuwa na mapafu yenye nguvu kama ya simba kutokana na alivyoweza kupaza sauti yake mbali na bila kuachia pumzi.

Kutokana na wakati huo elimu kwa watoto wa kike kutotiliwa mkazo, Siti hakuwahi kwenda shule wala kuhudhuria mafunzo ya Koran (madrasa). Hivyo mnamo mwaka 1911 aliona ni bora ahamie mjini ili kubooresha maisha yake zaidi. Ujio wake wa mjini ulikuwa wa neema kwani alikutana na bwana mmoja wa kundi la 'mziki wa Taarabu la "Nadi Ikhwani Safaa" aliyeitwa Muhsin Ali. Katika kipindi hicho hilo ndilo lilikuwa kundi pekee la muziki wa taarabu lililoanzishwa na Sultani mpenda starehe na anasa bwana Seyyid Barghash Said. Kundi hili lilikuwa ni la wanaume peke yake , wanawake hawakuruhusiwa kujiunga na vikundi vya muziki kwa vile ilikuwa ikichukuliwa kama ni uhuni. Bwana Muhsin alikiona kipaji cha pekee cha Siti na hivyo akajitolea kumfundisha kuimba kwa kufuata vyombo vya muziki na lugha ya kiarabu. Baada ya hapo alikwenda kumtambulisha kwa wanamuziki wenzie wa "Nadi Ikhwani Safaa" ambao bila kusita wakaanza kufanya naye maonyesho mbalimbali katika jamii. Walipata mialiko mingi hasa kutoka kwa Sultani na matajiri wengine wa Kiarabu, pia katika maharusi na sherehe zingine mbalimbali, inasemekana ulifika wakati ambapo sherehe ilishindwa kufana kama Siti binti Saadi hakuwepo kutumbuiza. Siti alikuwa ni moto wa kuotea mbali na jina lake lilivuma kwa haraka sana hadi nje ya mipaka ya nchi na bara la Afrika. Na punde Siti alianza kufananishwa na 'Umm Kulthum', mwimbaji mahiri wa kike aliyetamba wakati huo kutoka Misri.

Kama nilivyosema moto wa Siti ulikuwa si wa kuusogelea karibu, mwaka 1928 kampuni ya kurekodi muziki ya 'Culumbia and His Master's voice' yenye makazi yake Mumbai India ilisikia umaarufu wa Siti binti Saadi na hivyo ikamwalika yeye pamoja na kundi lake kwenda kurekodi kwa lugha ya Kiswahili ili kujaribu kama muziki wake utauzika. Kampuni ile haikuweza kuamini jinsi muziki ule ulivyouzika kwa kasi kubwa kwani wastani wa santuri 900 ziliweza kuuzika katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo, na hadi kufikia 1931 santuri 72,000 zilikuwa zimeuzwa. Kutokana na kusambaa kwa santuri hizi, umaarufu wa Siti ulizidi mara dufu watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia walikuwa wakija Zanzibari kuja kumwona. Mambo yalizidi kuwa mazuri kwa Siti hadi ikafikia hatua kampuni ya kurekodi ya Columbia kuamua kujenga studio ya kurekodi muziki palepale Zanzibar maalumu kwa ajili ya Siti binti Saadi.

Hatua hiyo ya hadi kujengewa studio iliwaumiza wengi wenye wivu, hivyo wakaanza kumtungia nyimbo za kumkejeli ili kumshusha na hasa walitumia kigezo kwamba hana uzuri wa sura, nyimbo nyingi ziliimbwa lakini huu ndio uliovuma sana:-
  • Siti binti Saadi kawa mtu lini,
  • Kaja mjini na kaniki chini,
  • Kama si sauti angekula nini?

Na yeye kwa kujua hila za wabaya wake, akaona isiwe taabu akajibu shambulio namna hii:-

  • Si hoja uzuri,
  • Na sura jamali,
  • Kuwa mtukufu,
  • Na jadi kebeli,
  • Hasara ya mtu,
  • Kukosa akili.

Kwa kujibu shambulio hilo kwa namna yake aliwafunga midomo wale wote waliokuwa wakifuata fuata. Siti pia alikuwa ni mwanamke wa kwanza mwanaharakati katika kipindi chake, alitetea wanawake na wanyonge kwa ujumla, kwani katika kipindi chake watu matajiri walikuwa wakiwaonea masikini na walipofikishwa mbele ya haki waliweza kutoa hongo na kuachiwa huru halafu wewe uliyeshitaki ndiye unayefungwa.

Utunzi wake wa wimbi wa Kijiti ulimpatia sifa kubwa kwani ulikuwa ukielezea kisa cha kweli kilichomkuta mwanamke mmoja mgeni kutoka bara, mwanamke huyu alipofika alikutana na Tajiri mmoja ambaye alijifanya amempenda, hivyo akamchukua na kulala naye halafu baadaye akamuua. Tajiri yule alishitakiwa na bahati nzuri walikuwepo mashahidi wawili walioshuhudia tukio lile, lakini kwa vile ni Tajiri alitoa pesa na kesi ikawageukia wale mashahidi na kufungwa.

Siti akatoa wimbo huu :-

  • Tazameni tazameni,
  • Eti alofanya Kijiti,
  • Kumchukua mgeni,
  • Kumcheza foliti,
  • Kenda naye maguguni,
  • Kamrejesha maiti.

    Siti aliendelea kumwambia katika nyimbo zake kwamba asijethubutu kwenda Dar er Salaam kwa maana watu wenye hasira wanamsubiri na wameapa kwa ajili yake.

    Siti aliendelea na shughuli yake ya muziki hadi uzeeni, muda mfupi kabla ya kifo chake alikutana na mwandishi maarufu na mwanamashairi Shaaban Robert ambaye alimhoji na kuweza kuandika wasifu wake katika kitabu alichokiita " Wasifu wa Siti binti Saadi" wasifu unaosemekana kuwa ndio bora zaidi uliowahi kuandikwa katika fasihi ya Tanzania. Kitabu hiki kinatumika kufundishia shule za sekondari za Tanzania.

    Tarehe 8/7/1950 Siti binti Saadi alifariki dunia na kuacha pengo kubwa katika fani ya Taarabu. Ingawa pengo hilo haliwezi kuzibika lakini kuna watu wengi walioweza kuibuka na umaarufu wa kuimba taarabu kupitia kwake, mfano hai ni Bi Kidude.

    Hata baada ya kifo chake jina lake bado linatumika sana kama kielelezo cha ushujaa wake, Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania, kimetumia jina lake kulipa jina gazeti la chama chao "Sauti ya Siti". Hadi leo hii Siti hutumika kama kipimo cha kufundishia uimbaji wa Taarabu. Na anakumbukwa katika historia yake ya kuwa mwanamke wa kwanza Afrika mashariki kurekodi muziki katika santuri.

    09 January 2006

    Oprah Winfrey akimsaili Michael Jackson.

     


    Pamoja na kuwaletea wasifu wa kina mama mashuhuri katika blogu hii, nitakuwa nikiwaletea pia habari zao wakiwa kazini kila siku kulingana na nitakavyokuwa nikizipata. Kama wote tunavyomjua oprah na mambo yake, nimebahatika kupata mahojiano yake na Michael Jackson yaliyofanyika mwaka 1993, Oprah ndiye mtu wa kwanza kabisa kukubaliwa na Michael kumfanyia mahojiano. Hebu soma hapa umjue kwa undani zaidi mwafrika huyu. Picha hiyo ya Oprah ilipigwa mwaka 1957 akiwa na miaka mitatu tayari alikuwa akijua kusoma na kuandika. Posted by Picasa

    02 January 2006

    Bi Kidude.


    Ingawa anajulikana zaidi kwa jina la Bi Kidude, lakini jina lake halisi ni Fatuma binti Baraka. Bi Kidude ni msanii mkongwe na mahiri sana katika fani ya muziki, hususani muziki wa mwambao ambao hujulikana kwa jina la Taarabu. Muziki huu ambao asili yake ni Misri umekita sana katika mwambao wa Afrika Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.

    Fatuma binti Baraka au Bi Kidude, alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Tanzania visiwani Zanzibar katika familia ya watoto saba (7), Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanya biashara wa nazi zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar. Bi Kidude anasema hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile anahakika ni kabla ya vita kuu ya kwanza ya dunia. Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka tisini (90).

    Bi Kidude anasema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka kumi (10) na alijifunza kutoka kwa Msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo Sitti binti Saad. Anasema wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa wako karibu basi yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale Nyumbani kwa Bi Sitti, wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje, kule ndani Bi Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye huku nje alikuwa akimsikiliza kwa makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa akiimba. Aliendelea hivyo hadi akawa mahiri sana katika uimbaji.

    Alipokuwa na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania bara, baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930, huko aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake uimbaji.

    Bi Kidude hategemei kazi moja tu ya kuimba, pia ni mfanya biashara ya 'Wanja' na 'hina' ambavyo anavitengeneza yeye mwenyewe, pia ni mtaalamu wa matibabu kwa dawa za mitishamba na zaidi ya hayo ni Mwalimu mzuri sana wa 'Unyago' ameanzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote hakuna aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.

    Watu wanasema 'Utu uzima dawa' Bi Kidude ana upeo mkubwa sana wa akili kwani pamoja na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na tamaduni za kiarabu ambapo mwanamke anatakiwa wakati wote akiwa hadharani ajifunike, Bi Kidude aliliona hili katika upeo mwingine kwamba ni sheria tu ya kitamaduni toka arabuni, hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake, na sasa hivi anavaa kama Mtanzania na si kama mwarabu. Lakini hakubakia hapo alivunja na miiko mingine zaidi ya kutokunywa na kuvuta, Bi Kidude anakata maji kisawasawa na kuvuta tumbaku na jani, lakini pamoja na yote hayo bado sauti yake iko pale pale.

    Amekwisha tembelea nchi nyingi sana ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.
    Amekwisha pata tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Tamasha la filamu ya nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 tuzo ni ya maisha. Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX ilienda kwake.

    Nyimbo alizowahi kuimba ni pamoja na Muhogo wa jang'ombe, na anaimba kwa kiswahili na Kiarabu. Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Koran.

    Kwa mahojiano msikilize hapa.

    Mungu azidi kumpa maisha marefu bibi yetu.

    01 January 2006

    Bibi Anna Claudia Senkoro atufungulia mwaka.


    Jina Anna Senkoro si geni tena masikioni mwa Mtanzania yeyote yule, mama huyu ndiye mwanamke pekee aliyeamua binafsi kuthubutu kugombea nafasi ya kuliongoza taifa zima la Tanzania katika awamu ya nne. Kutokana na uthubutu wake nimemchagua kutufungulia mwaka si kwa sababu nyingine yoyote ile bali ni kwa UTHUBUTU aliouonyesha. Binafsi ninaamini katika kujaribu na siamini katika kuogopa au kusikilizia. Sijui wenzangu mnasemaje juu ya uchaguzi nilioufanya? kama kuna lalamiko lolote naomba lisisite kunifikia. Kwa asiyemjua kwa sura ndiye huyo hapo juu.