01 October 2007

Malkia Nzinga Mbande wa Angola.


Nikiwa katika harakati ya kukusanya habari za wanawake waliotia fora duniani, nimeona niirudishe habari hii niliyoiandika hapo nyuma 2005 wakati nikianza kublogu hii ni kuwapa fursa wale ambao hawakuweza kuisoma nao wapate kumfahamu mama huyu, haya endelea...

Kama ukibahatika sasa hivi kukutana na Mreno, wewe jifanye kama unamchokoza juu ya wanawake wa afrika kwamba hawana lolote na hawawezi lolote, uone atakavyokushangaa, na bila shaka atakutupia swali kwamba unaishi dunia gani wewe?

Wasomaji msishangae, kwani aisifiae mvua...imemnyea. Hii yote imetokana na mwanamke mmoja jasiri, shupavu, mwenye akili sana na asiyetaka kuonewa wala kudharauliwa, si mwingine ni Malkia Nzinga Mbande. Mwanamama huyu aliyezaliwa mwaka 1583 na kufa 1663, alikuwa ni mtoto wa chifu na aliishi kipindi ambacho biashara ya utumwa ndio ilikuwa imepamba moto kwelikweli, kwa bahati mbaya baba yake alifariki na hivyo kaka yake mkubwa bwana Ngola Ngoli Mbandi akarithishwa madaraka ya baba yake. Mm! kaka huyu bila shaka aliguna kwa kujua kabisa kasheshe analotakiwa alikabili la kuwazuia wareno kuingia nchini kwao, lakini afanyeje na yeye ndio mwanaume na kama inavyojulikana kwa wengi mwanaume anaweza kila kitu na daima si mwoga, ikabidi ayavae madaraka huku akijua kabisa yeye ubavu wa kukabiliana na wareno hana na ni
mwoga kufa.

Dada yake, Nzinga baada ya kuona kaka yake anasua-sua ikabidi amwambie, kaka ni lazima uchukue hatua juu watu hawa na kuwazuia kuingia kututawala, lakini kwa vile kaka yake alikuwa mwoga ikabidi amwombe dada yake amsaidie, mara moja bila kuchelewa mwana mama Nzinga akaanza kuchukua hatua za utekelezaji na akafanikiwa kuwashawishi wareno katika kuandika mkataba wa makubaliano ya amani.

Tarehe ikapangwa ya kuweka saini makubaliano hayo, Kaka mtu kwa woga akakataa kwenda hivyo ikabidi Nzinga amwakilishe, akaenda na watumishi kadhaa lakini walipofika ndani ya ukumbi Nzinga akagundua kwamba hakuwekewa kiti yeye kama kiongozi wa nchi yake isipokuwa gavana wakireno peke yake, mwanamama akaona dharau gani hii? mara moja akapiga kofi na mmoja wa watumishi wake akaja mbele yake na kuinama magoti na mikono chini, Nzinga akakaa juu yake, kwa hiyo suala la gavana kukaa kwenye kiti peke yake likawa ngoma droo. Gavana akamtizama yule mama bila kummaliza na kubaki na aibu ya kuzidiwa maarifa tena na mwanamke, bila shaka alibaki akijiambia duh! kumbe wanawake nao wamo!!!

Nzinga baada ya kugundua kwamba kaka yake si kiongozi mzuri na hawezi kila kitu, alimfunga na kujitangaza kwamba yeye ndiye atakayeshika nchi kinyume na desturi ya nchi yao kwamba mwanamke haruhusiwi kushika wadhifa wowote wa uongozi katika serikali, minong'ono ya hapa na pale ilitokea lakini haikufika mbali kwani Nzinga alithibitisha ujasiri wake kwa vitendo. Na ni hapo ndipo umalkia wake ulipoanzia.

Kwa muda wa miaka arobaini ya uongozi wake, wareno walishindwa kuitwaa Angola hadi alipofariki, mwanamama huyu alijulikana na kuogopwa sana na ulaya nzima kwa mbinu zake thabiti za kijeshi, alijulikana kama mwanamke mpiganaji, jasiri na mwenye akili.
Hebu fikiria wareno, pamoja na kuwa na silaha imara na za kisasa ukilinganisha na za Malkia Nzinga, lakini walishindwa kuiteka Angola hadi Malkia Nzinga alipokufa.

Huyu kweli ni mwanamke wa shoka, na nina amini kila mwanamke anaweza kuwa mwanamke wa shoka, pale atakapoamua kufanya jambo kwa moyo na kuondoa uwoga. Hapa duniani kila jambo linawezekana, tatizo liko kwetu sisi wenyewe kutanguliza woga na kutokutaka kusumbuka.